Habari
HALMASHAURI KUU YA CCM WILAYA YA GEITA YATEMBELEA MRADI WA MAJI WA MIJI 28.
Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Geita, wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Geita, Ndugu Barnabas Mapande, wametembelea Mradi wa Maji wa Miji 28 kwa lengo la kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati.
Wakiwa katika eneo la mradi, wajumbe walipokea maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa GEUWASA, Mhandisi Frank Changawa kuhusu hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wake na manufaa yanayotarajiwa kwa Wananchi mara utakapokamilika.
Baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya mradi wajumbe walieleza kufurahishwa na kiwango cha utekelezaji kilichofikiwa pamoja na ubora wa kazi zinazoendelea wakieleza kuwa mradi huo ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuboresha huduma za maji kwa wananchi.
Mradi wa Maji wa Miji 28 unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba 2026, na unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia upatikanaji wa huduma ya maji ya uhakika kwa wananchi wa Geita

